Namna ya swala ya mtume (s.a.w). na Namna ya kutawadha
Mtunzi:
Imam Sheikh Abdul Aziz bin Abdullah bin Baz
Mfasiri:
Yasini Twaha Hassani.
Kimerejewa na:
Yunus Kanuni Ngenda.
Abubakari Shabani Rukonkwa.
كيفية صلاة النبي صلى الله عليه وسلم وكيفية الوضوء
السواحلية
المؤلف:
سماحة الشيخ: الإمام عبد العزيز بن عبد الله بن باز (رحمه الله).
المترجم:
ياسين طه حسن
المراجع:
يونس كنون نغندا
أبوبكر شعبان ركونكوا.
بسم الله الرحمن الرحيم
Namna ya swala ya mtume (s.a.w) na Namna ya kutawadha.
Utangulizi:
Namshukuru Mwenyezi Mungu peke yake, rehema na amani zimwendee mja wake na Mtume wake Mtume wetu Muhammad pamoja na familia yake na Maswahaba zake.
Amma baad.
Haya ni maneno kwa ufupi yanayo bainisha namna ya swala ya Mtume (s.a.w), nimekusudia kuileta kwa kila Muislamu mwanaume na mwanamke ili ajitahidi kila atakae soma kitabu hiki amuige Mtume (s.a.w) kwa ajili ya kufanyia kazi maneno yake Mtume (s.a.w): (Swalini kama mlivyo niona nikiswali). Kapokea hadithi hii Imamu Bukhari.
Ni juu ya msomaji kufuata haya:
1: AUKAMILISHE UDHU.
Nako ni kutawadha kama alivyo amrisha Mwenyezi Mungu kwa kauli yake tukufu: (Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikonoyenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni...). (Al-Maida: 6).
Na kauli ya Mtume (s.a.w): (Haikubaliwi swala bila ya kujitwaharisha). Ameipokea hadithi hii Imamu Abuu Daud na Tirmidhiy, na akaisahihisha Shekh Al-baniy (r.h).
Na udhu unakuwa kama ifuatavyo:
1: Anuwie kutawadha ndani ya moyo wake bila ya kutamka niya, kwa sababu Mtume (s.a.w) hakutamka niya wakati wa kutawadha kwake wala ndani ya swala yake wala katika ibada yake yoyote, kwa sababu Mwenyezi Mungu anafahamu yaliyomo moyoni hakuna haja ya kumwambia anayotaka kuyafanya.
2: Kisha aseme: (Bismi LLah).
3: Kisha aoshe vitanga vyake mara tatu.
4: Kisha aingize maji mdomoni na kusukutua na kupandisha mengine puani na kuyatoa kwa mkono wake wa kushoto mara tatu.
5: Kisha aoshe uso wake kuanzia maoteo ya nywele mpaka chini ya kidevu kwa urefu, na sikio hadi sikio kwa upana mara tatu.
6: Kisha aoshe mikono yake kuanzia mwanzo wa vidole mpaka kwenye kongo mbili mara tatu, akianzia mkono wa kulia kisha wa kushoto.
7:Kisha apake kichwani kwake mara moja, alowanishe vitanga vyake vya mikono kisha apitishe kuanzia mwanzo wa kichwa chake mpaka nyuma ya kichwa chake kisha arejeshe alipoanzia.
8: Kisha apake masikioni kwake mara moja, aingize vidole vyake kwenye masikio yake na apitishe vidole gumba vyake nyuma ya masikio yake.
9: Kisha aoshe miguu yake kuanzia mwanzo wa vidole mpaka juu ya fundo mbili mara tatu, aanzie mguu wa kulia kisha amalizie wa kushoto.
Amesema Mtume (s.w.a): (Hawi yeyote miongoni mwenu anapotawadha na kukamilisha udhu kisha akasema: Ash-hadu anlaa iLaha illa LLahu wahdahu laa sharika lahu, wa Ash-hadu anna Muhammada abduhu wa rasuluhu, isipokuwa hufunguliwa kwa ajili yake milango minane ya pepo ataingia katika mlango anaoutaka). Kaipoke hadithi hii Imamu Muslim.
2: ANAESWALI AELEKEE UPANDE WA KIBLA.
Nayo ni Al-Ka'bab, sehem yoyote atakayo kuwepo kwa mwili wake wote akikusudia kwa moyo wake kitendo cha swala aitakayo miongoni mwa swala za faradhi au za Sunna, na wala ulimi wake usitamke niya, kwa sababu kutamka niya siyo sheria, bali ni uzushi kwasababu Nabii Muhammad (s.a.w) hakutamka niya wala Maswahaba (r.a), na aweke sitra mbele yake ikiwa ni imamu au anaswali peke yake, na kuelekea kibla ni sharti miongoni mwa masharti swala.
3: ATOE TAKBIRA YA UFUNGUZI WA SWALA.
Kwa kusema: Allahu akbar, macho yake yakiangalia sehem ya kusujudia.
4: ANYANYUE MIKONO YAKE WAKATI WA KUTOA TAKBIRA.
Aielekeze usawa wa mabega yake au usawa wa masikio yake ikiwa imeelekezwa upande kibla.
5: AWEKE MIKONO YAKE JUU YA KIFUA CHAKE.
Aweke kitanga cha mkono wa kulia juu ya kitanga cha mkono wa kushoto, au kitanga cha mkono wa kulia kishike kwenye maunganishio ya kitanga cha mkono wa kushoto, au mkono wa kulia uwe juu ya mkono wa kushoto, yote hayo yamethibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w).
6: NI SUNNA ASOME DUA YA UFUNGUZI WA SWALA.
Naya ni: (Allahumma ba'id bayni wa bayna khatwa'yaaya kama ba'adta baynal-mashriq wal-maghrib, Allahumma naqqini min khatwa'yaaya kama yunaqqa thaubul-abyadh mina ddanas, Allahumma ighsilni min khatwa'yaaya bil-ma'I wa thalji wal-baradi). Kapokea hadithi hii Imamu Bukhari.
Na akitaka atasema: (Subhanaka Allahumma wa bihamdika wa tabaraka ismuka wa taala jadduka wa laa ilaha ghairuka). Na akileta dua tofauti na hizo miongoni mwa dua za ufunguzi wa swala zilizo thibiti kutoka kwa Mtume (s.a.w) hakuna tatizo, na iliyokuwa bora zaidi asome dua hii kipindi Fulani na hii kipindi kingine, kwakufanya hivo ni kuzifanyia kazi dalili zote zilizo pokelewa, kisha aseme: (Audhu biLLahi mina shaytwani rajim bismi Llahi Rrahmani Rrahim), na asome Suratul-fat'ha kwa kauli ya Mtume (s.a.w): (Hana swala yule asiye soma Suratul-fat'ha). Kapokea hadithi hii Imamu Bukhari.
Na aseme baada ya kumaliza Suratul-fat'ha: Amiin. Aidhihirishe katika swala ya sauti na asiidhihirishe katika swala ya sauti, kisha asome alicho jaaliwa katika Qur-an, na iliyokuwa bora zaidi asome baada ya Suratul-fat'ha katika swala Adhuhuri na Laasiri na Ishaa sura za kati na kati, (zisiwe sura ndefu wala fupi). Na katika swala ya Alfajiri asome sura ndefu na katika swala ya Magharibi wakati Fulani asome sura fupi na wakati mwingine asome sura ndefu, kwakufanya hivo atakuwa amezifanyia kazi dalili zote zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w).
7: ARUKUU KWA KUTOA TAKBIRA.
Akiwa ni mwenye kunyanyua mikono yake usawa wa mabega yake au usawa wa masikio yake, kichwa chake kikiwa usawa wa mgongo wake na vidole vya mikono yake vikiwa vimetanuliwa juu ya magoti yake, na atulizane katika kurukuu kwake na aseme: (Subhana Rabbiyal-adhwim), na iliyokua bora zaidi ayaseme mara tatu au zaidi, na ni Sunna kusema: (Subhanaka Llahumma wa bihamdika Allahumma ighfirli).
8: AINUE KICHWA CHAKE KUTOKA KATIKA RUKUU.
Akiwa ni mwenye kunyanyua mikono yake usawa wa mabega yake au usawa wa masikio yake huku akisema: (Samia Llahu liman hamidah) ikiwa ni Imamu au akiwa peke yake, na aseme wakati wa kuinuka kwake: (Rabbana wa lakal-hamdu hamdan kathira twayyiba mubaraka fiyhi mil'a samawati wa mil'al-ardhi wa mil'a maa baynahuma wa mil'a maa shiita min shay'in baad). Ikiwa ni ma'muma atasema wakati wa kutoka katika rukuu: (Rabbana wa lakal-hamdu… hadi mwisho wa dhikri), na akizidisha kila mmoja miongoni mwao yaani Imamu pamoja na ma'muma na yule anayeswali peke yake: (Ahlu thanai wal-majid ahaqu maa qalal-abdu wa kulluna laka abdu, Allahumma laa mania limaa a'atwayta walaa mu'twiya lima manaata walaa yamfau dhal-jaddi minkal-jaddi), itakua bora zaidi kwa kuthibiti hayo kutoka kwa Mtume (s.a.w), na ni bora zaidi kurejesha kila mmoja mikono yake kifuani kama ilivyokua kwenye kisimamo kabla ya kurukuu, kwa kuthibiti yanayoonyesha jambo hilo kutoka kwa Mtume (s.a.w), kama ilivyo pokelewa katika hadithi ya Waili bin Hujr na Sahli bin Sa'ad (r.a).
9: ASUJUDU KWA KUTOA TAKBIRA.
Akiwa ni mwenye kutanguliza magoti yake kabla ya mikono yake ikiwezekana, na akiona uzito atangulize mikono yake kabla ya magoti yake akiwa ni mwenye kuelekeza vidole vya miguu yake na mikono yake kibla, na awe ni mwenye kubana vidole vyake vya mikono kwa kuvinyoosha, na akiwa ni mwenye kusujudia viungo saba: Bapa la uso pamoja na pua, na vitanga viwili vya mikono, na magoto mawili, na matumbo ya vidole vya miguu miwili, na aseme: (Subhana Rabbiyal-A'ala), ni sunna aseme maneno hayo mara tatu au zaidi, na ni sunna kuongezea maneno hayo: (Subhanaka Allahumma wa bihamdika Allahumma ighfirli). Na azidishe dua kwa kauli ya Mtume (s.a.w): (Mkiwa katika rukuu mtukuzeni Mwenyezi Mungu, na mkiwa katika sijda jitahidini kuomba dua mkiwa na yakini ya kujibiwa maombi yenu), na amuombe Mola wake yaliyo mazuri duniani na akhera, sawasawa ikiwa katika swala ya faradhi au ya sunna, na asikutanishe mikono yake na mbavu zake, wala tumbo lake na mapaja yake, wala miundi yake na mapaja yake, na anyanyue mikono yake (asibane kwapa zake) kwa kauli ya Mtume (s.a.w): (Tulieni katika sijda na wala asilaze mmoja wenu mikono yake kama mbwa anavyo laza mikono yake). Amepokea hadithi hii Imamu Bukharin a Muslim.
10: AINUE KICHWA CHAKE KWA TAKBIRA.
Aulaze mguu wake wa kushoto na aukalie, na ausimamishe mguu wake wa kulia na kuweka vitanga vyake vya mikono juu ya mapaja yake au kwenye magoti na aseme: (Rabbi ighfirli war-hamni wah-dini war-zuqni wa a'fini waj-burni), na atulizane kwenye mkao huo.
11: ASUJUDU SIJDA YA PILI.
Kwa kutoa takbira na atafanya katika sijda hiyo kama alivyo fanya katika sijda ya kwanza.
12: AINUE KICHWA CHAKE KWA TAKBIRA.
Na akae kikao kidogo kati ya sijda mbili, na huitwa kikao hicho kikao cha mapumziko nacho ni sunna, akiacha kukaa kikao hicho hakuna tatizo, hakuna dhikri wala dua katika kikao hicho, kisha asimame kuelekea katika rakaa ya pili akichegemea magoti yake ikiwa yawezekana na akiona uzito ataweka mikono yake chini, kisha asome suratul-fatiha na atakacho jaaliwa katika Qur-an baada ya kusoma suratul-fatiha, kisha afanye kama alivyo fanya katika rakaa ya kwanza.
13: IKIWA SWALA NI YA RAKAA MBILI.
Mfano wa swala ya alfajiri na ijumaa na idd atakaa baada ya kutoka kwake katika sijda ya pili akiwa ni mwenye kuusimamisha mguu wake wa kulia na kuulaza mguu wake wa kushoto na kitanga chake cha mkono wa kulia kikiwa juu ya paja lake la kulia, akiwa ni mwenye kukunja vidole vyote isipokua kidole cha shahada atakiinua wakati wa kusema (Ash-hadu an laa ilaha illa Llah), na akikunja kidole kidogo na kinachofuatia katika mkono wake wa kulia na akikutanisha kidole cha kati na kidole gumba na akainua kidole cha shahada, ni sahihi kwa kuthibiti aina hizo mbili kutoka kwa Mtume (s.a.w), na iliyo bora zaidi ni kufanya namna hii katika swala Fulani na namna nyingine katika swala nyingine, na aweke mkono wake wa kushoto juu ya paja lake la kushoto au kwenye goti lake, kisha asome tahiyatu akiwa chini kwa kusema:
(Attahiyyatu liLlahi wa sswalawatu wa ttwayyibatu assalamu alayka ayyuha Nnabiyyu wa rahmatu Llahi wa barakatuhu assalamu alayna wa alaa ibadi Llahi sswalihina ash-hadu an laa ilaha illa Llahu wa ash-hadu anna Muhammada abduhu wa rasuluhu, -kisha aseme- Allahumma swalli alaa Muhammad wa alaa a'li Muhammad kama swallayta alaa Ibrahim wa alaa a'li Ibrahim innaka Hamidun Majid, wa bariki alaa Muhammad wa alaa a'li Muhammad kama barakta alaa Ibrahim wa alaa a'li Ibrahim innaka Hamidun Majid), na atake hifadhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na mambo manne na aseme: (Allahumma inni audhubika min adhabi jahannama wa min adhabil-qabri wa min fitnatil-mahya wal-mamati wa min fitnatil-masihi Ddajjali), kisha aombe dua kwa anayo yatakamiongoni mwa kheri za dunia na akhera, na akiwaombea wazazi wake au waislamu kwa ujumla hakuna tatizo, sawasawa ikiwa ni swala ya faradhi au ya sunna, kwa ujumla wa maneno ya Mtume (s.a.w), katika hadithi ya Abdallah bin Mas'ud (r.a) alipofundishwa tahiyatu kisha achague dua anayoitaka aiombe, katika upokezi mwingine kisha achague maswala anayotaka, nah ii inakusanya yanayo mnufaisha mja duniani na akhera, kisha atoe salam upande wake wa kulia na upande wa kushoto kwa kusema: (Assalamu alaykum warahmatu Llah, Assalamu alaykum warahmatu Llah).
14: IKIWA SWALA NI YA RAKAA TATU.
Kama swala ya magaribi au rakaa nne za adhuhuri na ishaa atasoma tahiyatu iliyotajwa hapo juu pamoja na kumtakia rehma Nabii Muhammad (s.a.w), kisha atasimama kwa kuchegemea magoti yake akiwa ni mwenye kuinua mikono yake uswa wa mabega yake au masikio yake kwa kusema: (Allahu akbar) na ataikusanya mikono yake kifuani kama ilivyo tangulia, kisha asome suratul-fatiha peke yake, na akisoma sura nyingine katika rakaa ya tatu naya nne katika swala ya adhuhuri baadhi ya nyakati hakuna tatizo kwa kuthibiti yanayo onyesha hilo kutoka kwa Mtume (s.a.w), kutokana hadithi ya Abi Said (r.a), kisha atoe tahiyatu baada ya rakaa ya tatu katika swala ya magharibi na rakaa ya nne katika swala ya adhuhuri na laasiri na ishaa kama ilivyo tangulia katika swala ya rakaa mbili.
YALIYO YA SUNNA KUYATAJA BAADA YA SALAM.
Aseme: (Astaghfiru Llah) mara tatu, (Allahumma Anta Ssalam wa minka Ssalam tabarkta yaa Dhal-Jalali wal-ikram). Kabla ya kuwageukia watu ikiwa ni imamu, kisha aseme: (Allahumma laa ma'nia lima a'twayta wala mu'twiya lima manaata wala yanfau dhal-jaddi minkal-jaddi, laa haula wala quwwata illa biLlah, laa ilaha illa Llahu wala naabudu illa iyyahu lahu nneematu walahul-fadhlu walahu Tthanaal-hasan, laa ilaha illa Llahu mukhliswina lahu ddini walau karihal-kafiruna-kisha aseme-Subhana Llah mara 33, Alhamdu liLlah mara 33, Allahu akbar mara 33 na aseme kwa kutimiza idadi ya mia moja: Laa ilaha illa Llahu wahdahu laa sharikalahu lahul-Mulku walahul-hamdu wa Huwa alaa kulli shay'in qadir, na asome Ayatul-kursy, na Qul Huwa Llahu, na Qul audhu biRabbil-falaq, na Qul audhu biRabbi Nnas baada ya kila swala, ni sunna kuzisoma sura hizo mara tatu baada ya swala ya alfajiri na magharibi, kama ilivyo pokelewa kutoka kwa Mtume (s.a.w), na nyiradi zote hizo ni sunna wala siyo faradhi.
SUNA ZILIZO PANGILIWA.
Ni sheria kwa kila muislamu mwanamume na mwanamke aswali kabla ya adhuhuri rakaa nne na baada ya adhuhuri rakaa mbili na baada ya magharibi rakaa mbili na baada ya ishaa rakaa mbili na kabla ya alfajiri rakaa mbili, jumla zitakua ni rakaa kumi na mbili, na hizo huitwa sunna zilizo pangiliwa kwasababu Mtume (s.a.w) alikua anazihifadhi akiwa hayupo safarini, lakini akiwa safarini alikua haziswali isipokuwa sunna ya alfajiri na witri, kwasababu sunna ya alfajiri na witri Mtume (s.a.w) alikua anazihifadhi akiwa hayupo safarini na akiwa safarini, na iliyo bora zaidi ni kuziswali sunna hizi pamoja na witri nyumbani, na akiziswalia msikitini hakuna tatizo, kwa kauli ya Mtume (s.a.w): (Atakae swali rakaa kumi na mbili za sunna kwa usiku na mchana atajengewa nyumba na Mwenyezi Mungu kutokana na rakaa hizo peponi). Kapokea hadithi hii Imamu Muslim katika sahihi yake.
Na akiswali rakaa nne kabla ya laasiri na rakaa mbili kabla ya magharibi na rakaa mbili kabla ya ishaa baada ya adhana na kabla ya kuqimiwa swala ni vizuri, kwasababu yamethibiti yanayo onyesha hayo kutoka kwa Mtume (s.w.a), na Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi wa kuwafiqisha, na rehma na amani za Mwenyezi Mungu zimwendee Mtume wetu Muhammad bin Abdallah pamoja na familia yake na Maswahaba zake na watakao mfuata kwa wema hadi siku ya mwisho.